Mkuu wa mkoa Iringa mh. Ally Salum Hapi ametoa siku 90 toka tarehe 11 agosti 2018 kuhakikisha wazee wote wa mkoa wa iringa waliotambuliwa wanapewa vitambulisho vya matibabu bure.
Ameyasema hayo jana wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri ya wilaya mufindi na mji wa mafinga zilizoko mkoani iringa wakati wa ziara yake ya kwanza wilayani mufindi kwa ajili ya kujitambulisha.
“Na kwenye hili nimesema wazee wasiwafuate halmashauri kwenda kupewa hivyo vitambulisho bali halmashauri kupitia mganga mkuu na timu yake mtoke muwafuate wazee kata kwa kata muwaandikishe, muwaasajili na kisha muwapelekee vitambulisho mahali walipo”.
Aidha amewataka watumishi kutofanya kazi kwa mazoea bali watimize wajibu wao kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria na pia waongeze ubunifu katika kazi zao ili kuleta matokeo chanya na kusisitiza kwamba kazi yao ni moja tu kuhakikisha wanamsaidia Rais.
Awamu ya tano inazungumzia hapa kazi tu ni lazima watendaji watoke ofisini na kwenda kuwahudumia wananchi ili kutatua shida zao, kutenda haki na kuwa waadilifu.
“Pia ni lazima tuongeze juhudi za kukusanya mapato ya serikali kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili halmashauri zetu zote za mkoa wa Iringa zisishuke asilimia 90%”alisema mh. Hapi.
Hata hivyo mh. Hapi ametangaza kuanza kwa kampeni ya iringa mpya ambapo atazunguka tarafa zote ndani ya siku 18 na kufanya mikutano isiyopungua 03 kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi.
Akisoma taarifa ya wilaya, mkuu wa wilaya mufindi mh. Jamhuri David William amesema anaishukuru serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida katika wilaya yake.
Mwaka 2017/2018 wilaya ya mufindi ilipokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha tshs bilioni 6 na milioni 200 kwa ajili ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Halmashauri ya mji wa mafinga mwaka 2017/2018 wamekusanya tshs. bilioni 2.6 kati ya lengo la kukusanya bilioni 2.7 sawa na asilimia 84%
“Mbali na hivyo umetuelekeza pia tuandike andiko maalumu kwa ajili ya mradi mwingine wa kimkakati wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka mafinga mjini hadi Mgololo kilomita 80. tunaenda kutekeleza kwani barabara hiyo inapita kwenye viwanda vingi ndani ya wilaya yetu na itaamsha uchumi wa maeneo mengi sana katika wilaya yetu” alisema mh. Wiliam
Akitoa shukrani mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa mafinga mh. Charles Makoga alisema “yote uliyoyasema kwetu sisi ni maagizo tunakuahidi tunakwenda kutekeleza na ninaomba watumishi sasa tukaanze vizuri kuanzia leo”.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.