WAZIRI WA OR-TAMISEMI INNOCENT BASHUNGWA ATETA NA MAAFISA HABARI WALIO CHINI YA OFISI YA RAIS TAMISEMI-DODOMA.
“Suala la kutoa taarifa kwa wananchi ni jambo la lazima, hivyo tuhakikishe wananchi wanapata taarifa kuhusu nini Serikali inafanya, Miradi inayotekelezwa na Fedha zinazopelekwa kwenye kila Halmashauri na Mkoa wananchi wajue kwani ni haki yao, na uwezo wa kutoa taarifa hizo mnao Maafisa Habari wa Serikali”
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Innocent Bashungwa alipokuwa na kikao cha kimkakati katika utendaji wa kazi na Maafisa Habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi zilizo chini ya TAMISEMI jijini Dodoma.
Mheshimiwa Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya sita inatekeleza Miradi mingi kwenye kila sekta na wananchi wanatakiwa wapate taarifa hizo kwani ni haki yao, na kazi ikifanyika kwa asilimia 70% ya utoaji taarifa za Serikali nina uhakika wananchi watajua nini Serikali inafanya na wananchi watakuwa wamefikiwa kwa asilimia kubwa.
Ameongeza kuwa atahakikisha vifaa kwaajili ya utendaji kazi vinapatikana kwa kila mikoa na Halmashauri ili utendaji kazi uwe mzuri wenye kutimiza matakwa ya wananchi na Serikali kwa ujumla wake na kwa mwaka huu mpya wa fedha amesema anatamani kuona utendaji kazi na upashaji wa habari za Serikali kwa Umma umeongezeka.
Kikao hicho cha siku mbili kimehudhuriwa na Msemaji Mkuu wa Serikali bwana Gerson Msigwa ambaye nae amewaasa Maafisa Habari kuongeza kasi ya utoaji wa habari na kuwa wabunifu katika njia mbalimbali za upashaji habari.
Wakurugenzi wa TAMISEMI wa Afya, Elimu, Tehama, Habari, Utumishi na Maafisa wengine waandamizi Ngazi ya Mkoa wa Dodoma na TAMISEMI wamehudhuria kikao hicho.
Imeandaliwa Ofisi ya Habari na Mawasiliano- MAFINGA TC
Sima Bingileki
Afisa Habari Mkuu
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.