Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe Joseph George Kakunda ameitaka bohari ya dawa na vifaa tiba (MSD) kupeleka vifaa tiba mara moja katika kituo cha afya Ihongole kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa.
Ameyasema hayo leo alipotembelea kituo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na kukagua jengo la maabara na chumba cha upasuaji (Theatre)
Mh. Kakunda ameiagiza bohari ya dawa na vifaa tiba (MSD) kuhakikisha wanapeleka vifaa tiba haraka iwezekanavyo na kutoa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha vifaa na madawa yanayotakiwa katika kituo hicho yanafika kwa wakati ili huduma muhimu zilizokusudiwa zianze kutolewa kwa wananchi.
“kituo chetu kimejengwa vizuri sana kwa viwango vyetu vya kitaifa, nimekagua chumba cha upasuaji nimeona kiko tayari kabisa kuanza kazi bado vifaa tiba tu” alisema Mh. Kakunda.
Aidha aliwapongeza mkuu wa wilaya, mkurugenzi na wakuu wa idara kwa usimamizi mzuri, “kazi hii imefanyika vizuri sana mimi kwa kweli napeleka ujumbe kwa Mhe Makamu wa rais aliyeweka jiwe la msingi kwamba kituo kimekamilika vizuri hongereni sana” alisema Naibu Waziri Mh. Kakunda.
Upanuzi na ukarabati wa kituo cha afya Ihongole ulipangwa kutumia kiasi cha shilingi milioni mia tano ambazo zote zimetolewa na Serikali kuu.
Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi novemba 2017 mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni mia nne themanini na tano ambazo ujenzi na ukarabati upo kwenye hatua za umaliziaji, fedha iliyobaki kiasi cha shilingi milioni kumi na tano itatumika kuweka mfumo wa GOTHOMIS pamoja na umaliziaji wa malipo ya kazi ndogo ndogo zilizobakia.
Hali ya utoaji huduma katika kituo cha afya Ihongole ni nzuri na imeendelea kuimarika hususani baada ya kuongezeka kwa fedha zinazotumika kununua dawa.
Akisoma taarifa ya upanuzi wa kituo mganga mfawidhi wa kituo cha afya Ihongole bi. Proserpina Kalanje alisema lengo la mradi huo ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na kinamama wajawazito kwa kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma za Afya katika kituo ili kiweze kutoa huduma za upasuaji wa dharula na huduma ya kuongeza damu.
“Ili kufanikisha hilo mradi umelenga kuongeza majengo ya upasuaji, maabara na wodi ya wazazi lakini pia tuna changamoto ya uhaba wa watumishi kwani mpaka sasa kituo kina watumishi kumi na sita tu wakati mahitaji ni arobaini na tisa hivyo tunaiomba serikali kutuongezea watumishi ili wananchi waendelee kupata huduma bora zaidi” alisema bi. Kalanje.
Kituo hiki kilianza kutoa huduma mwaka 2008 ambapo kilikuwa kinahudumia wastani wa watu 5,000 kwa mwaka na kwa sasa kinahudumia wastani wa watu 26,032 kwa mwaka ikiwa ni ongezeko la wastani wa watu 21,032 kutoka katika kata jirani za kinyanambo, changarawe na isalavanu.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.