VIVUTIO VYA UTALII
HISTORIA FUPI YA BAADHI YA VIVUTIO VIKUBWA VILIVYOPO KATIKA HALMASHI YA MJI WA MAFINGA.
Halmashauri ya mji wa mafinga ilikuwa ni sehemu ya halmashauri ya wilaya ya Mufindi, na ilitangazwa rasimi kuwa halmashauri inayojitegemea mwaka 2015, ni moja kati ya halmashauri tano za mkoa wa iringa, Inapatikana km 80 kusini mwa manisipaa ya Iringa. Halmashauri nyingine ni Mufindi, Iringa vijijini, Iringa mjini na Kilolo, Kusini na magharibi imepakana na halmashauri ya Mufindi, kasikazini imepakana na Iringa vijijini.
Mafinga mjini inapatikana kwenye latitude ya 800’S kusini mwa Ikweta na longitude ya 3500’E mashariki mwa Greenwich.
Wenyeji wa asili wanaopatikana katika halmashauri ya Miji wa Mafinga ni Wahehe lakini kwa sasa kuna mchanganyiko wa makabila mengi kutoka maeneo mbalimbali Tanzania.
RAMANI YA MKOA WA IRINGA IKIONYESHA MJI WA MAFINGA ULIPO
2.0 VIVUTIO VILIVYOPO
Baadhi ya vivutio vya kitalii vinavyopatikana ndani ya Halmashauli ya Mji wa Mafinga Wilayani Mufindi ni pamoja na Mapango ya Ulole yaliyotumika na mtwa mkwawa wakati wa vita, Uwepo wa eneo oevu lenye madhari ya kuvutia ambalo pia ni chanzo kikubwa cha mto Ruaha mkuu, Misitu mikubwa ya kupandwa inayochagiza uwepo wa hali ya hewa ya kipekee Wilayani Mufindi na uwepo wa kabuli la chifu Mnyigumba baba wa mtwa Mkwawa ambalo linabeba historia ya familia hiyo ya kichifu na kabila la wahehe kwa ujumla.
Pichani ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa mafinga pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wakiwa juu ya mapango ya ulole.
2.1 MAPANGO YA ULOLE
Mapango ya ulole yanapatikana mkoa wa Iringa wilaya ya Mufindi Halmashali ya mji wa Mafinga Kata ya bumilayinga, Kijiji cha Ulole, Kitongoji cha Nyawenzi kilometa 25 kutoka Mafinga Mjini.
Mapango haya yana urefu unaokadiriwa kuwa mita 700 kutoka lango la kuingilia mpaka lango la kutokea.
Mapango ya ulole ni sehemu iliyojengeka na mawe kiasili, kihistoria mapango ya ulole yanabeba mila na desturi za baadhi ya koo la kabila la wahehe ni sehemu ambayo inaaminika kuwa Mtwa Mkwawa na wafuasi wake walitumia kupumzikia pamoja na kupanga mikakati mbalimbali wakati wa mapigano mbalimbali yaliyohusisha kulinda himaya yake kwa ujumla. Inaaminika kuwa Mtwa mkwawa alitumia mapango hayo kama sehemu yakupanga mikakati yake ya Kumpiga Mngoni mwaka 1870’s, pamoja na wakati wa vita ya wahehe na wajerumani mwaka 1890’s.
Kwasasa mapango hayo hutumika kama sehemu ya kufanyia matambiko.
Pichani ni lango kuu lakuingia ndani ya mapango ya ulole ni sehemu inayosemekana kwamba maadui wa mkwawa (Wangoni) walitumia kuwasha moto mkubwa wa kuni wakiamini watawateketeza wanajeshi wa mkwawa waliokuwa ndani ya Pango
Mapango hayo ya ulole yanamuonekano wa asili na wakavutia sana toka nje ya mapango mpaka ndani ya mapango. Unapoelekea ndani ya mapango mita chache kutoka yalipo mapango kuna uoto wa asili wenye mchanganyiko wa aina mbali mbali za miti ya kiasili pamoja na milima na mabonde yanayopendezesha madhari ya eneo hilo, ukifika kwenye mapango hayo upande wa nje kuna muunganiko wa mawe mithiri ya mlango, ambapo ndipo Mtwa mkwawa na majeshi yake walitumia kama njia kuelekea ndani ya mapango hayo. Ndani ya mapango kumejengeka vyema mithiri ya ghorofa na kuna vyumba mbalimbali vilivyojengeka kiasili, pia ambavyo mtwa mkwawa na watu wake walitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Ndani ya mapango pia kuna mto wa maji ambao una madhari ya kipekee na muonekano wa ajabu, Mto huo wa maji unapita juu ya baadhi ya vyumba vilivyomo ndani ya mapango hayo, kitu kinachofanya mapango hayo kuonekana ya kipekee naya ajabu zaidi kuwahi kutokea. Baadhi ya vyumba ndani ya mapango kuna vitu vya asili kama vyungu na mabaki ya silaha za jadi ambazo inasemekana zilitumiwa na Wanajeshi wa Mkwawa wakati wa vita.
Mbali na kufurahia madhari ya mapango hayo, Ukifika kitongoji cha Nyawenzi utakutana na ukoo wa Kilingo ambao kimila ndo waliokabidhiwa eneo hilo na wanahistoria nyingi zaidi za kuvutia kuhusiana na mapango hayo.
Mapango ya ulole inaonekana kuwa kivutio kikubwa sana cha utalii unaohusisha asili na maeneo ya hatari yaani (ADVENTURE TOURISM) kutokana na muundo, ukubwa na maajabu ya mapango hayo, ila bado hayajawekewa miundo mbinu yakukionesha kama kivutio cha utalii na kama sehemu ya asili ya kujivunia kama taifa.
2.2 MAPENDEKEZO YA UBORESHAJI WA MAPANGO YA ULOLE
Mkoani Iringa wilaya ya Mufindi, halmashauri ya Mji wa Mafinga katika kata ya Rungemba takribani kilometa 10 kutoka stand kuu ya mabasi iliyopo Mafinga mjini, ndipo lilipo kaburi la chifu maarufu wa kihehe chifu Mnyigumba Mwamuyinga(Baba mzazi wa Mtwa Mkwawa) na ndipo vilipo viashiria vya uwepo wa masalia ya koo hizo za kina Myinga, ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya historia nyingi za ndani juu ya chimbuko lao tunaweza kuzipata hapo.
Pichani ni Kaburi la chifu Mnyigumba mwa Myinga na aliyesimama ndani ni Ignas Pangiligosi Mwamuyinga, almaarufu kama Malugila Mwamuyinga, ambaye ndiye aliyekabidhiwa masuala ya kimikla ya koo ya Mnyigumba kwa sasa.
Rungemba ni kijiji ambapo chifu Mnyigumba alizikwa baada ya kufariki, japo ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia ya kabila la wahehe na uchifu licha yakuwa ndipo yalipo kuwa makazi na ndipo alipozikwa chifu Mnyigumba bado jina lake halina umaarufu kama ambavyo wengi wangetarajia.
Lilipo kabuli hilo la Mnyigumba ni rahisi kukutana na wanaukoo wa chifu Mnyigumba ambao wanaweza kukupa historia ya koo yao japo nao historia hio wameitoa kutoka kwa wazazi wao.
Ukifika Rungemba kwa lengo la kutembelea kaburi hilo kwa sasa lazima utakutanishwa na moja ya wanafamilia wa Mnyigumba anayeitwa Ignas Pangiligosi Mwamuyinga, almaarufu kama Malugila Mwamuyinga, ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, ambaye muda wote huona fahari kuisimulia historia ya ukoo wao huo maarufu. Maligila ndiye mwanafamilia aliyekabidhiwa majukumu yote ya kimila kuhusiana na koo yao hiyo.
Wakati wa safari kuelekea kaburini kutokea kijijini ambapo ni kilometa 4 kutoka barabara kuu ya Iringa Mbeya kabla ya kufika kaburini kuna baadhi ya Nyumba za kale zilizobomoka ambazo inasemekana ndipo walipokuwa wakiishi baadhi ya wanaukoo na wafuasi wa chief Munyigumba. Nje ya Magofu hayo kuna mawe yenye kutu ambayo inaaminika ndipo wanajeshi wa Munyigumba walitumia kunoa na kutengenezea silaha zao za jadi, Kutu hiyo ipo miaka yote na haina dalili ya kupotea.
Malugila anasema “Mapagale” Nyumba ya kale iliyopo kwenye hayo mawe ni ya moja ya wafuasi wa Mtwa mkwawa aliyefahamika kama Bonamutwa, moja ya wafuasi waliomunusuru Mkwawa kuuwawa na Mjerumani kwa kumficha kwenye gara la kuhifadhia nafaka “Kihenge” na walipo fika wajerumani kumuulizia akawaambia kuwa ni kweli amepita maeneo hayo ila amemwambia anaenda kwa chifu wa Usangu Nyemele.
Na licha ya kuona kaburi wanafamilia wanauwezo wa kutoa historia ya chimbuko la kizazi chao ambacho ndicho kimebeba koo nyingi za kabila la wahehe na katika ziara ya Idara ya maliasili Malugila alidokezea kwa ufupi historia ya chimbuko lao.
Malugila anatuambia “Shina la ukoo wao linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia(Mhabeshi)” Malugila anaendelea kutuambia alichosimuliwa na mababu zake “Mufwimi alikuwa ni kutoka Ethiopia aliye kuwa akizunguka akiwinda huku na kule na kutokea Ethiopia, alifika Kenya akiwa kwenye shughuli zake za uwindaji kabla ya kuingia Tanganyika na kufika Usagara hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia ilipokuwa himaya ya Chifu Mwamududa.
Mufwimi inasemekana alikuwa mwindaji mzuri wa mnyama aina ya nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, baadae Mfwimi alimpelekea zawadi ya nyamachoma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Ukaribu wake na chifu wa himaya hiyo uliongezeka na akapendwa sana na kukaribishwa na chifu Mwamududa kuishi kwake.
Mapenzi hayajaanza leo wala jana, mapenzi hayachagui, mapenzi yanajenga taswira ya ujasiri kupita kiasi mda mwingine, baada ya mda mfupi Mfwimi alimpenda motto wa chifu na kuanzisha mapenzi ya siri na mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Semduda, Binti huyo baadae akapata ujauzito. Roho ya wooga ikamuingia Mufwimi, akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa kwa chifu mduda kwa kumpa mimba mwanae. Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kuwa anamuogopa baba ake hivo yeye anaondoka, lakini akamuomba ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi. Muyinga Mufwimi ni msemo wa kihehe unaomaanisha Mwindaji Muhangaikaji. Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba inakosemekana aliuawa na nyati na mpaka leo hakuna ajuaye lilipo kaburi lake. Lakini kumbe hali ilikuwa tofauti kwa mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa bintiye angekubali kuolewa kutokana na kuwakataa wanaume wengi hapo awali waliokuwa wakimchumbia. Na kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameombwa kufanya na baba wa mtoto huyo Mufwimi mwenyewe.
Muyinga Mufwimi alipokua, Kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugila. Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, Na katika utawala akabahatika kupata watoto watatu wa kiume nao ni Maliga, Nyenza na Mpondwa.
Maliga naye akabahatika kupata watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe. Katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa. Mudegela Maliga naye baadae akabahatika kuwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Chifu Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia watoto wawili ambao ni Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa mke mwingine wa pili mdogo ake na mke wa kwanza aliyewazaa Gunyigutalamu, akaoa mdogo wao mwingine na wake zake wa awali aliyeazaa akina Mupoma, Magoyo Magidanga, Mhalwike, na Magohaganzali. Chifu Kilonge alipofariki alizikwa katika Kijiji cha Lupembe lwa Senga, ambapo kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, japo Pembe hizo ziliibiwa baada ya muda na inasemekana walioshiriki wote kwenye wizi wa hizo pembe walifariki mmoja baada ya mwingnine muda mfupi tu baada ya tukio hilo.
Kama tulivoona awali Mnyigumba alikuwa ni mtoto wa pili kwa mke mkubwa wa chifu Kilonge, na kama yalivyo mambo ya utawala wakichifu mara nyingi mtoto mkubwa wa kiume ndiye aliyekuwa akirithishwa utawala, Kwa maana hiyo Mnyigumba alihofia kuukosa uchifu ambao inaonekana alikuwa ashaanza kuutamani. Utawala una mambo mengi sana hauna tofauti yoyote na siasa zetu za sasa , Mwaka 1860 inasemekana Mnyigumba alifanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye aweze kurithi utawala kutoka kwa baba ake. Lakini kipindi Mnyigumba anafanikisha kumuua kaka yake, Kaka yake alikua tayari ana mke aliyejulikana kama Sekinyaga. Kama ilivo kuwa kwa mila za kihehe kaka akifariki mke wake alikuwa akirithishwa kwa ndugu au mdogo ake na marehemu hivyo ye mwenyewe Mnyigumba akamchukua Sekinyaga kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, inasemekana tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
Na baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto. Kwa hiyo kwa historia hii tu Malangalila Gamoto siyo mtoto wa Munyigumba kama wengi wanavyosema , bali ni wa kaka yake Ngawonalupembe, ingawa Munyigumba ndiye aliyemlea. Lakini baadae inasemekana ugomvi ulitokea baina ya Munyigumba na mkewe huyo wa kurithi baada ya mama huyo kuamua kumwambia Munyigumba kuwa huyu siyo mtoto wake bali ni wa kaka ake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe japo kiuhalisia inaonekana Munyigumba alijua toka awali na alitamani iwe siri ili kumlindia heshima kwa jamii anayo itawala.
Inaelezwa kwamba alipofukuzwa tu, Sekinyaga alielekea maeneo ya Mufindi kasikazini kwenye kijiji cha Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi na kudhamiria kumrudisha tena mwanamke huyo kwenye himaya yake. Ila wafuasi wake aliowatuma kumufuata huyo mama wakaenda kumuua huko huko Sadani. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake wenye baba tofauti lakini babu yao ni mmoja.Munyigumba alikuwa na jumla ya wake watano ambao ni Sengimba, Sendale, Sekinyaga, Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mke wa kwanza alibahatika kupata watoto watano ambao ni Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale yeye alipata mtoto mmoja ambae ni Mgungihaka; Sengimba mdogo wake mke mkubwa yeye alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga yeye aliishia kumzaa Gamoto kutoka kwa kaka yake Munyigumba.
Uongozi wa Munyigumba mtoto wa chifu Kilonge Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tu tangu alipomuua kaka yake Ngawonalupembe mwaka 1860. Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika Kijiji cha Rungemba.
Chifu Munyigumba ni kati ya machifu waliofanikisha kuunganisha koo nyingi sana na kuziweka pamoja na kuzifanya kama jamii moja. Mpaka anafariki chifu Mnyigumba alikuwa amefanikisha kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo zilizozaa kabila la Wahehe, wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni mtoto wake wa kwanza, alikuwa na umri wa miaka 24.
Hii ni sehemu tu Ndogo yahistoria ya chifu Mnyigumba ambayo imejificha kwa ukubwa kijijini Rungemba walipo baadhi ya wanaukoo wa Mnyigumba mwamyinga.
Heshima ya chifu Mnyigumba pamoja na mwanae mtwa Mkwawa kimataifa ni kiashiria tosha cha kuifanya Rungemba kuwa kitovu cha utalii wa historia ya kabila la wahehe ambalo kwa ukubwa limeunganishwa na chief Mnyigumba enzi za uhai wake.
3.1 MAPENDEKEZO YA KUBORESHA UTALII KATIKA KABULI LA MNYIGUMBA
4. HITIMISHO
Hivi ni baadhi ya vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Halmashauri ya Mji wa mafinga ambako ndipo chimbuko la Mtwa Mkwawa.Vivutio hivi bado havijafahamika sana hivyo juhudu za makusudi zinahitajika ili kuvitangaza vivutio hivyo.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.