“Tumepitisha bajeti hii hakikisheni mnaisimamia, hiki kiwe ni kiapo chenu na sisi tutawahukumu kwa hili msipoitekeleza.Mmeiandaa wenyewe na mhakikishe mnaitekeleza. Pia miradi yote mnayoianzisha hakikisheni mnaikamilisha kwa wakati na thamani ya fedha iendane na miradi husika. Tuepuke kuanzisha miradi mizigo isiyotekelezeka”
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri cha Wilaya
( DCC) kwaajili ya kupitisha Mpango wa Bajeti ya Halmashauri ya Mji Mafinga kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yenye thamani ya TSH 29,312,377,819.00.
Akiwasillisha Taarifa mbele Kamati hiyo, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu Ndugu, Apolinary Seiya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi, Happiness Laizer amesema kuwa katika fedha hizo,
- Bilioni 6.790 ni kwaajili ya Miradi ya Maendeleo
-Bilioni 16.539 Mishahara
-Bilioni 5.982 Matumizi mengineyo .
Ameongeza kuwa katika mapato hayo Halmashauri inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 6.283 mapato yake ya ndani ambapo Bilioni 1.388 ni mapato fungiwa na Bilioni 5.339 mapato Halisi.
Amevitaja vipaumbele vya Halmashauri vilivyojumuishwa kwenye Mpango na Bajeti wa mwaka wa fedha 2023/2024 kuwa ni:-
-Kuimarisha Utawala Bora kwa kuzingatia,demokrasia, Utawala wa sheria,
-Ukusanyaji wa Mapato
-Kutekeleza miradi mipya na kukamilisha miradi viporo katika sekta ya Elimu , Afya, Utawala na huduma za Jamii. Pia kuimarisha hali ya Usafi na mazingira.
Akichangia kuhusu miradi itakayotekelezwa katika bajeti hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mheshimiwa Cosato Chumi amesema kuwa Mji wa Mafinga unakuwa kwa kasi kubwa hivyo lengo ni kuhakikisha wananchi na wafanyabiashara wanafanya kazi katika mazingira mazuri hata nyakati za usiku kwa kuweka taa za barabarani.
Ameshauri kuongeza kwa ujenzi wa shule za mchepuo wa kingereza kwani, shule hizo zitaongeza ajira, wanafunzi watapata elimu kwa lugha ya kingereza kwa gharama ndogo na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Kikao cha kamati kimehudhuriwa na viongozi wa Chama na Serikali,watendaji wa kata viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi mbalimbali.
Sima Bingileki
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Halmashauri Ya Mji Mafinga.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.