Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Daud Yasin imefanya ziara ya kukagua Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Mji Mafinga ikiwa ni kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Miradi iliyotembelewa na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa ni Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Ifingo, Ujenzi wa Jengo la Dharura( EMD) na Mradi wa Maji wa Igowole.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua Miradi hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Daud Yasin kwaniaba ya wajumbe wengine wa Kamati hiyo amesema, Miradi yote ni bora na thamani ya Miradi na Fedha vinaendana na imekamilika kwa wakati hivyo itapunguza changamoto ya Maji na ubali wa kufuata huduma za Afya kwa wananchi wa Maeneo husika.
" Huu ndio Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi lazima tuhakikishe Miradi inakamilika kwa wakati kwani Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikileta fedha kwenye Halmashauri lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za Afya bora na kwa wakati, niwakumbushe tu watumishi wa Umma lugha tunazotoa kwa wananchi tunapowapa huduma wananchi ziendane na Ubora wa majengo haya” Daud Yasin Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa.
Akisoma taarifa kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Mji Mafinga, Dkt. Bonaventura Chitopela amesema kuwa Kituo cha Afya Ifingo kimejengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu kiasi cha Shilingi Milioni 650, Fedha kutoka Halmashauri shilingi Milioni 200 na Mchango wa Wananchi Shilingi milioni 12.
Amesema kituo hicho cha Afya kitaanza kutoa huduma mapema mwezi wa tatu mwaka huu na majengo ambayo yamekamilika ni jengo la Kupokea wagonjwa wa Nje, wodi ya wazazi, chumba cha Upasuaji, chumba cha kufulia nguo,njia za kupita wagonjwa na kichomea taka.
Ameongeza kuwa mpaka sasa kituo kimepokea vifaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mheshimiwa Cosato Chumi.
Vifaa vilivyopokelewa kutoka TAMISEMI ni
Meza ya Upasuaji, Taa ya Upasuaji na jokofu . Aidha vifaa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge ni vitanda 37 na magodoro 18.
Ziara pia imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Mji Mafinga.
IMEANDALIWA NA :
Sima Bingileki
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.