MAFINGA TC MSHINDI WA PILI USAFI WA MAZINGIRA 2022 KUNDI LA HALMASHAURI ZA MIJI KITAIFA.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Seif Shekilaghe kwa Niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameitangaza Halmashauri ya Mji Mafinga kuwa Mshindi wa Pili katika Usafi wa Mazingira kundi la Halmashauri za Miji Kitaifa kwa mwaka 2022 na kupokea zawadi ya Cheti na Fedha Shilingi Milioni Kumi.
Dr. Seif amesema kuwa Usafi wa Mazingira uwe ni Agenda ya kudumu kwa ngazi ya familia na ngazi ya jamii kwani kila mmoja akishajua kuwa Usafi ni lazima itakuwa ni tabia ya jamii nzima. Hii itapelekea jamii kufanya Usafi kama tabia bila kusubiri Mashindano.
“Natamani kujua hivi haya Mashindano yasipokuwepo je? Itakuwa ndo mwisho wa jamii kuhamasishwa kuwa na vyoo bora? Sisi kama viongozi tujue tuna wajibu kufanya usafi kama agenda kuanzia ngazi ya jamii.”
Akizungumza baada ya kupokea ushindi huo Mwenyekiti wa Mji Mafinga Mheshimiwa Regnant Kivinge amesema pongezi za dhati ziende kwa Mkurugenzi wa Mji Bi, Happiness Laizer kwa usimamizi wake bila kuchoka usiku na mchana kuhakikisha Mji wa Mafinga unakuwa safi.
Amempongeza pia Afisa Afya wa Mji Mafinga Gaudience Haule, Idara ya Afya, Usafi wa Mazingira na watumishi wote kwa kuhakikisha Mji unakuwa safi na kupanga mikakati ya kuboresha Usafi kwa ngazi ya Mtaa, Kata hadi Wilaya.
Halmashauri ya Mji Mafinga imeshinda kundi la Halmashauri za Miji ambapo Mshindi wa Kwanza ni Babati, Mshindi wa Pili ni Mji Mafinga na Mshindi wa Tatu ni Mji Njombe.
Kwa mwaka 2022 Wizara ya Afya ilitenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwaajili ya zawadi kwa washindi ambapo mashindano yamehusisha makundi 11.
Wiki ya Usafi wa Mazingira ilianza rasmi huko Singida lengo likiwa ni kuchochea jamii kushiriki katika Usafi na kuboresha Mazingira kuanzia ngazi ya jamii.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI- MAFINGATC
Sima Bingileki
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano-Mafinga Tc
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.