Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. David Cosato Chumi (Mb.), amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Bw. Amin Mawji.
Mhe. Chumi amepokea Hati hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Mhe. Chumi amempongeza Bw. Mawji kwa uteuzi wake huo na kumuahidi kuwa Wizara itampatia ushirikiano wakati wa kutekeleza majukumu yake.
Pia, Mhe. Chumi aliipongeza AKDN kwa mchango mkubwa katika jitihada za kupambana na umaskini, kuimarisha elimu, kuboresha huduma za afya, na kurejesha utamaduni Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wake, Bw. Mawji ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya AKDN na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo, hasa katika maeneo ya kupambana na saratani Afrika Mashariki, utafiti wa mabadiliko ya tabianchi, na hifadhi ya mazingira kwa kushirikiana na vyuo vikuu ndani na nje ya nchi, kama vile Canada na Ujerumani.
Bw. Mawji anachukua nafasi ya Bw. Amin Kurji, ambaye anamaliza muda wake kama Mwakilishi Mkazi wa AKDN nchini.
Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ni Shirika la Kimataifa linalojitolea kuboresha maisha ya watu hasa barani Asia na Afrika, bila kujali asili, dini au jinsia.
AKDN imefanya kazi nchini tangu mwaka 1991 na inatekeleza miradi yake katika nchi mbalimbali duniani.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.