Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia, Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) itajenga kituo cha kutoa taarifa za utalii za Ukanda wa Kusini mwa Tanzania katika eneo la Kihesa Kilolo Mkoani Iringa.
“Ujenzi unatarajiwa kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 18. Zabuni ya Ujenzi wa Mradi imetangazwa tarehe 5 Septemba, 2023 na Mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi unatarajiwa kusainiwa mwanzoni mwa Mwezi Novemba, 2023.
Ujenzi wa kituo utakuwa wa miezi 12.”
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Angellah Kairuki ( Mb) alipokuwa akizindua maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2023 katika viwanja vya Kihesa Kilolo Iringa tarehe 23/9/2023
Amesema Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Balozi na kinara namba moja wa kukuza Utalii na Uwekezaji nchini kupitia Kampeni ya Tanzania The Royal Tour” hivyo lazima tumuunge Mkono Mheshimiwa Rais kwa kutangaza vivutio vya Utalii na kuvuta Wawekezaji ili kukuza na kuongeza Pato la Taifa.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 Sekta ya Utalii imevunja rekodi kwa kuwa na ongezeko ambalo halijawai kutokea, kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 jumla ya watalii 1,638,850 waliliingizia Taifa jumla ya Shilingi bilioni 522.7 ikilinganishwa na watalii 1,123,130 walioingizia Taifa Shilingi bilioni 290.4 mwaka wa fedha 2021/2022. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 45.9 ya watalii na mapato ya asilimia 80
Akitoa taarifa ya Maonesho ya Utalii Karibu Kusini Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Dendego amesema Mikoa 10 kutoka nyanda za juu Kusini ndio waratibu wa Maonesho haya na jumla ya washiriki 130 wameshiriki. Viongozi mbalimbali wa wakiwemo, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, wakurugenzi, viongozi wa Taasisi pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wameshiri uzinduzi wa Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2023 mkoani Iringa.
Maonesho ya Utalii Karibu Kusini yalianza rasmi mwaka 2019 ambapo mpaka sasa ni mzunguko wa nne tangu kuanza kwake. Kwa mwaka huu 2023 maonesho yatakuwa kwa siku 5 kuanzia tarehe 23-27.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.