Mkutano maalumu wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji Mafinga limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na kuidhinisha kukusanya na kutumia zaidi ya Bilioni 25.2 kwa ajili ya matumizi ya mishahara, mengineyo na miradi ya maendeleo.
Akisoma rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Andambike Kyomo amesema zaidi ya Bilioni 3.9 zinakadiriwa kukusanywa kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya Halmashauri.
Makisio hayo ni zaidi ya milioni 648.8 ambayo ni asilimia 20% ukilinganisha na makisio ya mwaka 2018/2019 ya zaidi ya Tsh bilioni 3.3, aidha katika mapato hayo kiasi cha zaidi ya Tsh milioni 602.8 ni mapato ya vyanzo fungiwa katika idara ya afya na elimu sekondari hivyo kufikia mapato halisi kuwa zaidi ya bilioni 3.3.
Baraza hilo limeridhia pia matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo zaidi ya bilioni 17.8 zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mishahara , kati ya fedha hizo kiasi cha zaidi ya Tsh bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara, na zaidi ya bilioni 4 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Aidha baraza hilo limeidhinisha pia kukusanya na kutumia zaidi ya bilioni 7.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kati ya fedha hizo zaidi ya bilioni 4.7 ni kutoka ruzuku ya Serikali kuu, wahisani zaidi ya milioni 490, Halmashauri inatarajia kuchangia zaidi ya bilioni 1.3 sawa na asilimia 40 ya mapato halisi ya ndani ya Halmashauri na nguvu ya wananchi wanatarajia kuchangia zaidi ya milioni 768.
Akieleza matarajio ya utekelezaji wa rasimu ya bajeti hiyo ya 2019/2020 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina ametanabaisha kwamba bajeti hiyo italenga kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na kuongeza mapato ya ndani, kuongeza viwanda na fursa za uwekezaji, kuboresha huduma za usafi katika mji, kuboresha makazi na mipango miji sanjari na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na vitendea kazi na hatimae kukamilisha miradi viporo iliyoanzishwa siku nyingi katika sekta ya afya, elimu utawala na ujenzi.
Akiongoza baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amewahakikishia wananchi wa Mafinga kwamba bajeti hiyo iliyoidhinishwa leo hii itaenda kutekelezwa ipasavyo na imelenga kutatua kero za wananchi.
“Sisi kama watekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi wote kwa pamoja kwa kushirikiana na madiwani wa chadema kwa pamoja tunashirikiana kuhakikisha bajeti hii inaenda kutekelezwa katika kata zetu zote kama iliyopangwa bila kujali vyama vyetu kwani maendeleo hayana chama” Alisema
Aidha ameeleza kwamba katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt John Magufuli za kuleta elimu bure na matokeo chanya yanayotokea ya ongezeko la wanafunzi, Halmashauri yake imejiandaa kuongeza kujenga shule mbili za Sekondari mpya ikiwemo ya vipaji maalumu na nyingine ya Wasichana itakayojulikana kwa jina la Mafinga Girls hii ni kutokana na ongezeko la ufaulu wa mtihani wa darasa la saba ambapo halmashauri hiyo imefikia asilimia 92.86% ya ufaulu kwa mwaka 2018 na kushika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Iringa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Mufindi Kaimu Katibu Tawala (DAS) Bwana Joseph Mchina ameipongeza Halmashauri ya mji wa Mafinga kwa kuwa na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Waheshimiwa Madiwani endeleeni kushirikiana na wataalamu hawa wa Halmashauri na wananchi kwa ujumla katika kufanikisha utekelezaji wa miradi yetu kwa viwango vyenye ubora unaotakiwa ambavyo thamani yake ya fedha inaonekana ili kuchochea maendeleo ya wananchi na kufikia kipato cha kati kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho” Alisema.
Mafinga Town.
Postal Address: Po.Box 76 Mafinga
Simu: +255 262 772 393
Mobile: 026-2772393
Barua Pepe: td@mafingatc.go.tz
Copyright ©2018 Mafinga Town Council . All rights reserved.